Biblia inafundisha nini kuhusu vipaji vya Kiroho?

Mwandishi: 
Jari Rankinen
Mtafsiri: 
Richard Ondicho Otiso

Vipaji vya kiroho ni nini?

Kipaji cha kiroho, kinachoitwa pia karisma, ni nguvu au talanta ya ajabu inayotolewa na Roho Mtakatifu. Kuna vipaji vingi vya kiroho. Katika Biblia tunapata mifano yake: karama ya uponyaji, uwezo wa hekima, kunena kwa ndimi, kutabiri, kufundisha, hamu ya kuwahudumia wengine, uwezo wa kuongoza kanisa, hamu ya kutoa na hamu ya kuwasaidia maskini, uwezo wa kutofautisha wakati Roho wa Mungu anazungumza na wakati ni roho mchafu, na kadhalika. (Warumi 12:6–8, 1 Wakorintho 12:8–10, 1 Wakorintho 12:28–30, Waefeso 4:11, 1 Petro 4:11).

Hivyo hii ni mifano ya karama za kiroho. Biblia haikusudia kutoa orodha kamili yake. Tunaweza kusema kwamba karama zote zinazokuwezesha kutumikia ufalme wa Mungu na kusaidia kanisa la Mungu kutimiza ujumbe wake katika ulimwengu huu ni vipaji vya kiroho.

Tayari tumepokea baadhi ya vipaji vya kiroho wakati Muumba wetu alipotufanya na kututayarishia karama fulani. Kwa mfano, ubunifu wa muziki au uwezo wa kuongoza au kufundisha ni moja ya hizi. Unapotumia ujuzi wako kwa ajili ya kanisa, ni sahihi kuviita vipaji vya kiroho. Baadhi ya vipaji havihusiani na vipaji vyetu vya asili, vya kuzaliwa navyo. Kwa mfano, kunena kwa ndimi ni uwezo wa aina hiyo, unaoelekea kuwa wa "miujiza" zaidi, unaotolewa na Roho Mtakatifu. Wewe pia una kipaji cha kiroho. Kinaweza kuwa uwezo wa kawaida sana. Tumia ujuzi wako kutumikia ufalme wa Mungu, na ndio kipaji chako cha kiroho.

Katika sura ya kumi na mbili ya Wakorintho ya Kwanza, maneno mawili ya Kiyunani yanatafsiriwa kama vipaji vya kiroho: neno pneumatika ("vitu vya Roho") na karisma. Neno karisma linatokana na neno "charis", ambalo maana yake ni "neema". Neno hilo linaeleza jambo muhimu kuhusu vipaji vya kiroho. Havitolewi kulingana na ustahili, kwa sababu hapo vingekuwa vipaji vya ustahili. Vipaji vya kiroho vinatolewa kwa neema. Roho Mtakatifu wa Mungu anatoa anachopenda kwa kila mtu, na hatujui kwa nini Yeye anagawia kila mmoja kama anavyopenda.

"Haya yote ni kazi ya Roho mmoja huyo, naye hugawia kwa kila mmoja kama apendavyo."
(1 Wakorintho 12:11)

Hii pia ndiyo sababu Wakristo hawapaswi kupangwa kwa mujibu wa vipaji gani mtu anayo. Paulo hata anasema kwamba Mungu huwafunika waumini wa chini wa kanisa kwa utukufu mkuu. Wale ambao hawapokei kipaji cha thamani hawahitaji - wao ni muhimu katika kanisa hata hivyo (1 Wakor. 12:24).

Vipaji vya kiroho si sharti la imani ya kweli

Imani ya kweli si pale tu ambapo kuna vipaji vya kiroho. Na si mtu aliye na kipaji fulani cha kiroho pekee ndiye anaye imani ya kweli. Injili ya Yesu aliyesulubiwa inatosha kwa imani ya wokovu, na hakuna kingine kinachohitajika, hata vipaji vya kiroho.

Hii ni lazima isisitizwe hasa katika makanisa yale ambapo Mungu ametoa vipaji vingi vya kiroho vinavyoelekea kuwa vya "miujiza". Vinaweza kuanza kutarajiwa kwa kila mtu. Pia kuna daima wale waumini wa kanisa ambao wanahisi kwamba hawana vipaji vya kiroho na kwa hiyo wanahisi kuwa duni. Ni muhimu basi kujua hili: Hata kama huna vipaji vyovyote vya kiroho na hata kama hujui chochote kuhusu vipaji vya kiroho, unaweza kumwamini Yesu. Na katika imani kwa Bwana aliyesulubiwa una kila kitu unachohitaji kuishi kama mwana wa Mungu na kufika mbinguni.

Wahubiri wengine wanafundisha kwamba kuna aina mbili za Wakristo: Kuna wale walio na Roho Mtakatifu na ambao wana kipaji cha kiroho kama ishara ya hili (kawaida wanasema kwamba kipaji hiki ni kunena kwa ndimi). Pia, kuna Wakristo wale ambao bado hawajapokea Roho Mtakatifu, lakini wanapaswa kujitahidi kufika kiwango ambacho nao watapokea Roho wa Mungu. Tunakataa mafundisho kama hayo, kwa sababu Biblia haifundishi chochote kama hicho.

Watoto wote wa Mungu wana Roho Mtakatifu. Ishara kwamba mtu amepokea Roho wa Mungu ni kwamba anaamwamini Yesu. Hakuna mtu anayeweza kumwamini bila Roho Mtakatifu.

Kujazwa na Roho, ambayo Biblia inazungumza, ina maana kwamba Roho wa Mungu, anayeishi ndani yetu, anachukua nafasi zaidi na zaidi katika mioyo yetu. Tunamwomba Mungu hili litokee kwetu.

Kuishi kama mwana wa Mungu si sana juu ya nguvu na miujiza, bali ni juu ya kubeba msalaba ambao Mungu amempa kila mmoja wetu. Kubeba msalaba ni udhaifu, ugonjwa, matatizo, kudharauliwa au ukweli kwamba muujiza uliotegemewa haukutokea. Na wale ambao maisha yao ni kama haya si watoto wabaya wa Mungu. Kulingana na neno la Mungu, wao ni wapendwa hasa kwa Mungu.

Vipaji vya kiroho si dhamana ya imani ya kweli

Hata pale ambapo Mungu wa utatu (Baba, Mwana na Roho Mtakatifu) hajulikani au pale watu humkana, baadhi ya watu wanazungumza kwa ndimi au wagonjwa wanaweza kuponywa. Na hata Shetani anaweza kufanya miujiza. Yeye anapotosha kwa ufanisi zaidi hasa pale ambapo vitendo vyake vinafanana na vitendo vya Mungu.

Na wakati mwingine Mungu anafanya kazi kwa njia ya ajabu: Anaweza kutoa vipaji vya kiroho kwa makanisa yale ambayo katika mambo mengine yanafundisha na kuishi kinyume na neno lake. Kanisa la Wakorintho lilikuwa mfano wa hili. Paulo analisifu kanisa kwa kuwa na vipaji vingi tofauti vya kiroho na hasemi kwamba vipaji si kutoka kwa Mungu. Na bado Paulo ni lazima ashughulikie upizani mwingi na neno la Mungu na anaonya kwamba kama kanisa halitatubu katika haya, litahukumiwa wakati Bwana atakapokuja.

Uwepo wa vipaji vya kiroho haupaswi kutupotosha kufikiri kwamba kila kitu ni sahihi na jema pale ambapo vipaji vya kiroho vinatumika. Vipaji vya kiroho si ishara kwamba Mungu sasa amekubali kitu fulani - ambacho, hata hivyo, ni kinyume na Biblia. Hivyo, uwepo wa vipaji vya kiroho haupaswi, kuwa mfano, kutuongoza kushirikiana na wale wanaofundisha kubatiza tena wale waliobatizwa wakiwa watoto wachanga. Wanaweza kuwa na neema zilizotolewa na Mungu na bado wanafundisha kuhusu ubatizo kinyume na neno la Mungu. Neno la Mungu linatuonya pia sisi: Tutahukumiwa kama vipaji vya kiroho vitatupofusha ili tuanze kufundisha na kutenda kinyume na neno la Mungu.

Omba vipaji vya kiroho na uvitumie

Biblia inatuambia tufuatilie vipaji vya kiroho. Biblia inasema ukweli rahisi: Wale wanaoomba wanapokea. Wale wasioomba wanabaki bila. Kufuatilia si kushinikiza - kushinikiza Mungu au kushinikiza mtu mwingine. Ni maombi ya unyenyekevu.

Je, tumekuwa tukifuatilia vipaji vya kiroho? Kuanzia sasa, je, hatuwezi kuomba kwa sauti, kwa mfano, katika mkutano wa kanisa, kwamba Mungu angetupatia vipaji vya kiroho ambavyo kanisa letu linahitaji. Maombi pia yangefungua njia kwa matumizi ya vipaji vya kiroho. Ni busara kumwomba Mungu atupe kile anachojua tunahitaji. Inaweza kuwa kitu tofauti kabisa na kile tunafikiri sisi wenyewe.

Biblia inakataza kuficha vipaji vya kiroho. Hivyo tumia kipaji chako - hata kama kipaji chako ni cha namna kwamba unaona aibu nayo kwa namna fulani au wengine hawakithamini. Mungu hajatoa kipaji bure. Kanisa linakihitaji.

Weka msalaba wa Yesu katikati ya imani yako

Jambo muhimu zaidi katika imani yetu ni kile Yesu alichofanya kwa ajili yetu msalabani. Jifunze kutegemea hilo peke yake. Jifunze kutotegemea kile ulicho. Jifunze kutotegemea kile unachoona Mungu ametimiza kwako, au kama umepokea kipaji cha kiroho au jinsi unavyokitumia. Hili ni jambo gumu na kwa hiyo lazima tujifunze jambo hili.

Msalaba wa Yesu ndio msingi wa kudumu pekee. Unasimama hata siku zile ambapo huoni kitu chema ndani yako au hata wakati kipaji hicho cha kiroho kimepungua au kimezimika kabisa. Na hata katika siku hizo, msalaba wa Yesu una kila kitu unachohitaji kwa wokovu wako na kuishi kama mwana wa Mungu. Kama imani yetu inategemea kitu kingine, msingi wake utaporomoka. Na inatokea kwa haraka ya kushangaza.

Kama kipaji cha kiroho kinaongoza maisha ya imani ili kitu kingine zaidi ya msalaba wa Yesu kiwe jambo muhimu zaidi, kipaji hicho cha kiroho kinatumika vibaya. Pia ni kweli kwamba kwa wengi ni hasa kipaji cha kiroho ambacho kimefanya upya uhusiano wao na Yesu na kumfanya msalaba wake uwe wa kupendwa zaidi.

Upendo wa Mungu unaonyeshwa kupitia vipaji vya kiroho

Paulo anafundisha katika barua ya kwanza kwa Wakorintho kwamba vipaji vya kiroho ni vya thamani tu pale ambapo upendo unaonyeshwa kupitia hivi - upendo ambao Yesu pia alitupenda nao. Kama matumizi ya kipaji cha kiroho ni kuwadharau wengine, kufuatilia maslahi yako mwenyewe na kuwasahau wengine, ni, kulingana na maneno ya Paulo, sawa na mtu kupiga ngoma mara kwa mara. Wengi husikia sauti, lakini haina faida. Na inaumiza masikio.

Basi, je, kipaji chako kinakuongoza kutegemea zaidi na zaidi kwa uthabiti wa msalaba wa Yesu yake? Je, unawaongoza wengine kwa Bwana aliyesulubiwa kwa kipaji chako? Je, unapenda kipaji chako? Je, unatumia kipaji chako kwa manufaa ya wengine? Juta kama hujatumia kipaji chako kama hivi. Lakini usifiche kipaji chako. Kuanzia sasa, mwombe Mungu ujuzi na unyenyekevu wa kupenda kipaji chako na kutukuza msalaba wa Yesu. Hata kwa kipaji kidogo cha kugusika, unaweza kupenda na kutukuza maana ya kazi ya Yesu msalabani, na hapo kipaji hicho ni cha thamani zaidi. Kwa upande mwingine, hata kipaji cha kujionyesha kinaweza kutumika kwa madhumuni ya ubinafsi, na kipaji kama hicho hakina thamani.

Kipaji kinachotumika kwa unyenyekevu hujenga kanisa vizuri zaidi. Kiburi na kujiweka juu ya wengine inadhoofisha kanisa vibaya.

Biblia na vipaji vya neema

Mungu hazungumzi kupitia vipaji vya kiroho kinyume na anachosema katika Biblia. Unabii hauwezi kupindua neno lililoandikwa la Mungu. Kama na wakati kuna unabii unaopingana na Biblia, hauitoki kwa Mungu. Hata mtu wa imani anaweza kutangaza unabii kama huo, na pia mhubiri kama vile tulivyozoea kumwona kama mwalimu wa kuaminika. Hivi ndivyo dhambi inavyoweza kuonekana kwetu. Yeyote, kulingana na unabii kama huo, anayelazimisha kuamini na kutenda kinyume na Biblia, anamwinua mtu mahali pa Mungu na yuko katika hatarini kubwa ya kupotea kutoka njia ya mbinguni.

Roho Mtakatifu anafanya kazi hasa katika neno la Biblia. Ndio maana vipaji vya kiroho vilivyozaliwa na Roho wa Mungu vinatuambatisha zaidi na zaidi kwa neno la Mungu. Swali hili - je, kipaji cha kiroho kinafanya Biblia iwe ya kupendwa zaidi - ni kwa kweli kiashiria kizuri cha kipaji ni kutoka kwa Mungu au la, na kama kipaji kinatumika vizuri. Watu wengi wanasema kwamba kipaji cha kiroho kiliwapa shauku mpya ya kusoma Biblia na nguvu ya kuitenda. Lakini maisha ya mtu fulani yanaonyesha kwamba kipaji kinakupeleka mbali na neno la Mungu. Kipaji kama hicho hakiwezi kutoka kwa Mungu. Au kipaji kilichotolewa na Mungu kinatumika tofauti na jinsi Mungu alivyokusudia.

Sisi ni tofauti

Vipaji vya kiroho vinavutia baadhi ya watu kujiunga na kanisa. Wengine wanawafukuza. Rafiki yangu ambaye alitokea kuwepo katika tukio ambapo ndimi zilizungumzwa na kutabiriwa alisema, "Kama imani kwa Yesu ni kama hii, sitaki lolote kuhusu imani." Paulo pia anajua uwezekano huu, na ndio maana anawaaambia kutumia vipaji kwa hekima. Hatupaswi kumfukuza mtu yeyote kutoka kwa Yesu. Kwa hiyo, baadhi ya vipaji lazima vitumike kwa uangalifu na wakati mwingine hazipaswi kutumika. Na kwanza kabisa, vipaji vya kiroho lazima vizungumzwe na kufundishwa - ili viwe vya kawaida na si vya kutisha - na ni baada tu ya mafundisho ndipo vinavyoweza kutumika.

Sisi ni tofauti. Mmoja ana mtazamo wa hisia kali kwa imani na anatamani uzoefu katika maisha ya kidini. Wengine wanapima mambo ya imani kiakili na hawahitaji sana uzoefu. Mungu ameumba utu wa kipekee ndani ya kila mmoja wetu. Mazingira yetu na hatua katika njia ya kidini ni tofauti. Na hii inaathiri jinsi tunavyohisi kuhusu vipaji vya kiroho. Ni lazima turuhusu tofauti hii ya uzoefu wa kibinadamu. Neno la Mungu pia linaruhusu. Lakini kila mtu ni lazima aamini na atende kulingana na neno la Mungu.