1 Yohana 2 – Utukufu wa Mungu na mwenye dhambi

Mwandishi: 
Erkki Koskenniemi
Mtafsiri: 
Richard Ondicho

Soma au sikiliza Waraka wa Kwanza wa Yohana mtandaoni (Neno Bibilia Takatifu SNT, Bible Gateway)


Tulipoangalia sura ya kwanza ya waraka huu, tuliona kwamba mgawanyo wa sura (ambao haukufanywa na mwandishi mwenyewe) katika Biblia unakatiza mtiririko wa mawazo. Ndiyo maana mstari wa mwisho wa sura ya kwanza uliachwa ili kushughulikiwa hapa. Hebu tupitie muundo wa sehemu hii tena. Taarifa kuu ni kifungu katika mstari wa tano, "Mungu ni nuru, na ndani yake hakuna giza hata kidogo." Kuweka mipaka kunaanza baada ya hii, kupitia maagizo yanayotokana na taarifa kuu – ni nini kinachokubaliana na utukufu wa ajabu wa Mungu na nini hakikubaliani. Hakikubaliani ikiwa tunadai kuwa wa Mungu lakini tunaishi katika dhambi (1:6-7), au ikiwa tunadai kwamba hatuna dhambi (1:8-9). Sasa tutaangalia agizo linalofuata, ambalo linatupeleka hadi sura ya pili.

Watoto wa nuru wanapambana na dhambi zao 1:10-2:2

Agizo la tatu katika sehemu hii linaonekana kurudia yale ya awali lakini, kwa kweli, linatupeleka mbali mbele. Mwanzoni, kuna ukosoaji kwa wale ambao, kimsingi, wanakubali kuwa wadhambi, lakini kwa kweli wanaikana. Ni rahisi kukubali kuwa mdhambi lakini ni vigumu zaidi kuungama matendo yetu maovu. Hata hivyo, ni jambo ambalo Mkristo lazima aendelee kufanya, au vinginevyo Mungu anafanywa kuwa mwongo. Mungu kwa kweli anasema kwamba sisi ni wadhambi na kwamba anatusamehe dhambi zetu kwa damu ya Kristo. Ikiwa tunadai kuwa safi, tunafanya njia ya msalaba ya Kristo kuwa bure kabisa na, wakati huo huo, ya uongo.

Katika sehemu ya mwisho, mwandishi anazungumza na "watoto" wake wapendwa, wapokeaji wa waraka. Msingi sasa umeimarishwa, na tunaweza kutoa hitimisho. Kisichokubaliana na utukufu wa Mungu ni dhambi, au kuikana dhambi yetu, au matendo yetu maovu binafsi. Ni baada tu ya kujifunza kuelewa ukweli huu na kujua utakatifu wa Mungu, udhambi wetu wenyewe, na upatanisho wa dhambi zetu kwa damu ya Mwana wa Mungu ndipo tunaweza kusikiliza onyo: pambana na dhambi! Dhambi ni kitu hatari na cha kutisha. Na bado, wakati huo huo, kuna pia faraja: ikiwa mtu yeyote anatenda dhambi – ambayo, kutoka sura ya kwanza na kutoka uzoefu wetu wenyewe, ni ukweli wa kudumu – tuna mtetezi kwa Baba. Yesu Kristo ndiye upatanisho wa dhambi zetu, na si kwa zetu tu bali pia kwa dhambi za ulimwengu wote.

Mtoto wa nuru anapenda amri za Bwana 2:3-5a

Agizo la nne linatuambia kitu kile kile ambacho Bwana mwenyewe anasema kwa urahisi, "Mtawatambua kwa matunda yao." Kulikuwa na walimu wa uongo wanaodai kuijua njia ya Mungu vizuri. Maisha yao, hata hivyo, yalikuwa mfano wa onyo. Hayakuwa yanakubaliana na utukufu wa Mungu hata kidogo. Kwa hiyo, walimu kama hao walipaswa kukataliwa, na ilikuwa muhimu sana kuachana nao kabisa. Kwa mwalimu za kweli, amri za Mungu ni za thamani na za ajabu. Upendo kwa Yesu si kitu kisicho na maana, bali upendo huo unaonekana wazi katika jinsi tunavyoihusiana na neno lake.

Neno la Mungu pia hapa ni gumu sana. Lazima tujichunguze na kuinamisha vichwa vyetu. Tunakumbuka agizo lililotolewa awali: watoto wa nuru wasiikane dhambi yao kamili. Na, tukikabiliwa na maneno haya, itakuwa vigumu kuikana.

Tunapokea pia mafundisho yanayofaa sana kwa wakati huu. Kuna walimu wengi, wenye kusadikisha, wanaovutia, wenye vipaji. Inaonekana ya kushangaza kwamba maisha ya mtu anayefundisha neno la Mungu si suala la kibinafsi. Kinyume chake kabisa, sisi kama wanachama wa kanisa tunashauriwa kuangalia jinsi walimu wanavyoishi. Kipimo tunachopewa si upana wa tabasamu zao, au jinsi wanavyoinama kwa ustadi, bali ni jinsi maneno ya Mungu yanavyoonekana kupendwa katika maisha ya mwalimu mwenyewe. Swali ni kuhusu heshima yao kwa mistari halisi ya Biblia. Ikiwa maisha ya walimu hayastahimili uchunguzi katika suala hili, wanabatilisha mahubiri yao kwa maisha yao wenyewe, na hakuna mtu anayepaswa kuwasikiliza.

Watoto wa nuru wanafuata mfano wa Bwana katika maisha yao 2:5b-8

Yohana anaendelea kupiga kwa nguvu na anafanya uzushi wa walimu wa uongo kuanguka kama nyumba ya karatasi. Wanadai kumjua Mungu vizuri kwa uzoefu na maarifa yao wenyewe. Yohana anakataa hili kwa njia ya moja kwa moja sana. Yeyote anayemilikiwa na Bwana anapaswa kuweka upendo wa kujitoa wa Yesu kama mfano kwake mwenyewe. Kwa kuwa hakukuwa na ishara ya hili, mafundisho yao yalikuwa ya makosa. Walimu wa uongo walikuwa wamewapatia watu mambo mapya ya kuvutia. Yohana, kwa upande mwingine, anatoa amri ya kale na rahisi sana: ishi ukifuata mfano wa Kristo!

Tunaweza tena kuona hapa, jinsi imani ya Kikristo si kitu cha kinadharia na kigumu. Ni rahisi sana: tunaishi katika neema na upendo wa Mungu, tunasikiliza neno lake, na tunatubu ipasavyo. Imani yetu si ngumu zaidi ya hii. Na bado inajumuisha kujifunza na kusoma ambako kutadumu milele na milele.

Watoto wa nuru hawamchukii jirani yao 2:9-11

Mwandishi anaendelea kueleza zaidi, akiacha nafasi ndogo ya kutoelewana. Swali ni, tunawatendea vipi jirani zetu? Yeyote anayedai kuwa wa Mungu lakini, wakati huo huo, anamchukia jirani yake, anaonyesha kwamba anasema uongo. Pia, yeye mwenyewe anaweza kufikiri kwamba yeye ni mtoto wa nuru lakini, kwa kweli, bado anaishi gizani. Yeyote anayetembea gizani amepotea na hana wazo tena yuko wapi au anakwenda wapi. Giza limempofusha macho yake, na hatapata tena njia sahihi. Mambo ni tofauti kabisa kwa yule anayempenda jirani yake. Ni kazi inayokubaliana na utukufu wa Mungu. Mtu kama huyu kwa hiyo pia atabaki kama mtoto wa nuru.

Maneno ni magumu na yanazidi kuwa magumu. Hatupaswi kujaribu kuyalainisha na kuyaeleza. Hivyo ndivyo Biblia inavyoeleza mambo. Bila shaka. Labda sasa tunaelewa kwa nini tunaoonywa kuhusu hukumu ya mwisho na, hasa, kuhusu hatari ya kupokea hukumu ya Mungu kwa nguvu zetu wenyewe tu. Kimbilio letu pekee ni kwamba dhambi zetu zimesamehewa kwa damu ya upatanisho ya Kristo. Vifungu hivi vikali vya Biblia vinatufundisha kutoa hitimisho sahihi kutokana na ukweli kwamba sisi ni wa Mungu.

Kanisa linalindwa vizuri 2:12-14

Yohana anajua kwamba amezungumza kwa ukali na imara. Alikuwa akiwafikiria kwanza na zaidi walimu wa uongo ambao walikuwa wamepanda mbegu za sumu. Sasa ni wakati wa kufariji. Mistari hiyo imefasiriwa kwa njia moja katika Biblia yetu, lakini labda lazima ieleweke hivi, "Ninawaandikia, watoto wadogo, kwamba dhambi zenu zimesamehewa kwa jina lake." Tunapata hapo mfuatano wa ajabu unaoshuhudia neema ya Mungu na unaelekezwa kwa wasomaji wa waraka. Si onyo hapa bali ni taarifa: dhambi zimesamehewa kwa damu ya Mwana wa Mungu. Tunaposhiki imani hii, yule mwovu ameshindwa.

Mafundisho ya uongo ni mitego ya shetani. Mafundisho sahihi, ya kimitume yanatuzuia kuanguka ndani yake. Utukufu wa Mungu ni mkubwa wa kushinda, na usiku wa ulimwengu ni giza totoro. Mwenye dhambi yuko salama tu katika kanisa la Kristo, lakini yuko salama kabisa hapo, katika utunzaji wa neno la kimitume.

Usipende ulimwengu! 2:15-17

Imani katika Kristo ni kitu ambacho tunatoa hitimisho katika maisha yetu ya kila siku. Tunajikuta mara kwa mara katika hali ambapo lazima tufanye uchaguzi kuhusu ni nini muhimu zaidi kwetu. Ama tunampenda Baba Mungu au ulimwengu huu. Yesu anasema kitu kile kile hivi, "Hazina yako ilipo, hapo moyo wako utakuwako pia." Je, nitajisalimisha kwa tamaa yangu ya dhambi na kwa mambo ambayo ulimwengu huu unayatoa, au nitakumbuka kwamba mimi ni mtoto wa Mungu? Hii inamaanisha Ukristo wa vitendo.

Waraka wa kwanza wa Yohana unatusaidia katika hali zetu za kufanya uchaguzi: ulimwengu huu na vyote vilivyomo vitapita siku moja. Ikiwa hiyo ni hazina yetu, sisi wenyewe tutapita pamoja na ulimwengu huu unaoweza kuharibika. Ikiwa Bwana ni hazina yetu, kwa neema yake, tutaishi milele na milele.

Wapinga-Kristo na siku za mwisho 2:18-25

Wale walio wa Mungu hawaishi nje ya ufikiaji wa yule mwovu katika ulimwengu huu. Kwa njia ya uongo na mafundisho ya uongo, shetani anatafuta mawindo. Yohana anazungumza kuhusu mpinga-Kristo kwanza kwa umoja na kisha kwa wingi. Kuja kwa mpinga-Kristo ni ishara ya wakati wa mwisho. Wakati waraka ulipoandikwa, kulikuwa na "wapinga-Kristo" wengi. Walikuwa Wakristo wa zamani, lakini si Wakristo wa kweli, ambayo ilithibitishwa na kuanguka kwao. Walitambulika kama wapinga-Kristo kwa sababu ya mafundisho yao. Kiini chake kilikuwa kwamba walimkana Yesu kama Kristo wa Mungu anayerejelewa katika Agano la Kale. Kuna mazungumzo zaidi kuhusu hili baadaye katika waraka. Yeyote asiyetaka kumjua Yesu hana Mungu pia. Yeyote aliye na Yesu ana Baba pia.

Mafundisho ya awali ya kimitume yatawaweka waumini kama warithi wa uzima wa milele. "Upako" unamaanisha hapa Roho Mtakatifu ambaye walikuwa naye tangu ubatizo wao mtakatifu. Zawadi hii kutoka kwa Mungu inawazuia kuanguka hadi mwisho wa ulimwengu.

Wakati mwingine tunasikia kitu kama hiki, "Mimi ninamwamini Mungu, lakini tunamhitaji Yesu kwa nini?" Ukristo bila Kristo unaonekana kukubalika zaidi kuliko mafundisho ya kimitume. Msalaba wa Bwana unapokutwa na ukimya kabisa na mazungumzo yakiwa kuhusu mambo ya kuvutia zaidi, kuna angalau mtu mmoja anayetaka kuisikiliza kanisa. Lakini hiyo ni njia ya kumpoteza si tu Kristo bali pia Baba! Njia pekee ya kwenda kwa Mungu ni kupitia mlango, na mlango huo ni Kristo. Hatutawasikiliza wale wanaopitisha "kisasa" Ukristo, wala, kwa sababu yoyote, wale wanaokana kwa utaratibu upatanisho wa dhambi zetu kwa Yesu (Wamormoni na Mashahidi wa Yehova).

Siku za mwisho zinajadiliwa sana. Kuja kwa mpinga-Kristo kunatolewa hapa kama ishara. Tunaweza pia kuona kwamba waraka ulipoandikwa, wakati wa mwisho ulikuwa bado haujafika, ingawa kulikuwa na wapinga-Kristo wengi. Kivuli kidogo cha mpinga-Kristo kilikuwa tayari kinaeneza giza lake katika huduma ya walimu wa uongo. Kivuli hiki kimeitia giza vipindi vingi katika historia. Mafundisho ya uongo, udanganyifu mkubwa, uasi, chuki kipofu, na mateso ya Wakristo ni ishara za nyakati za mpinga-Kristo. Katika wakati wetu wenyewe, tunaweza kuona ishara nyingi zinazoelekeza siku za mwisho. Ishara hizi zitaonekana kikamilifu tu muda mfupi kabla ya mwisho. Katikati ya wasiwasi, tutakumbuka kwamba baada ya dhiki kubwa, siku za mwisho zitatuleta ukombozi kamili.

Ninawezaje kubaki katika imani hadi mwisho? 2:26-27

Kanuni iliyoguswa awali inarudiwa katika sehemu hii: "upako", Roho Mtakatifu, atawaweka waumini kama wa Mungu na kuwaongoza kwenye ukweli wote. Walimu wa uongo hawaongozwi na Roho Mtakatifu. Ndiyo maana wanaeneza uongo tupu. Wasikilizaji lazima, kinyume na mafundisho yao, washike mafundisho waliyoyapokea kutoka kwa mitume. Mwandishi kwa hiyo anasema kwamba Roho Mtakatifu atawaweka waumini waaminifu.

Ni jambo la ajabu kujua kwamba kubaki na kuvumilia katika imani hakutegemei utendaji wetu wenyewe. Vinginevyo hatungekuwa na nguvu za kuishi. Lakini hatupaswi kusahau kwamba Roho Mtakatifu anatumia neno la Mungu kama chombo. Kwa hiyo, lazima tulisikilize, tulisoma, na kutubu ipasavyo.

Mistari ya mwisho ya sura hii (2:28-29) ni ya sehemu inayofuata. Kwa sababu hii, tutaijadili pamoja na sura ya tatu.