Waraka wa Tatu wa Yohana – Mwongozo wa Masomo

Mwandishi: 
Erkki Koskenniemi
Mtafsiri: 
Richard Ondicho

Soma au sikiliza Waraka wa Tatu wa Yohana mtandaoni (Neno Bibilia Takatifu SNT, Bible Gateway)


Barua kwa Gayo

Waraka wa Tatu wa Yohana unazungumzia masuala yale yale kama Waraka wa Pili wa Yohana, lakini mazingira ni tofauti kabisa. Waraka huu pia unahusu watembezi na kanisa la mahali fulani. Lakini sasa uongozi wa kanisa la mahali fulani hauko ktika mikono salama. Wakati huu watembezi, wanaojaribu kuboresha hali, wako sawa na si wenye makosa.

Gayo, mwanachama wa kutaniko anayefanya jambo sahihi 3 Yohana 1-4

Tofauti na Waraka wa Pili wa Yohana, waraka wa tatu haujaelekezwa kwa kanisa la mahali fulani. Mpokezi wa barua ni 'Gayo' ambaye 'mzee' anamwandikia. Mzee hahitaji kujitambulisha katika waraka huu, wala katika waraka wa pili. Yeye ni mtu anayejulikana katika eneo lake, na mamlaka yake hayana budi kupingwa.

Gayo ni jina la kwanza la Kiroma. Kulikuwa na idadi ndogo sana ya majina haya, na mengi yao yalikuwa ya kawaida sana. Kwa sababu hiyo, hakuna faida kujaribu kutafuta uhusiano wowote na Gayo wa Korintho, ambaye jina lake kamili labda lilikuwa Gayo Titio Yusto. Popote walipokuwepo raia wa Kiroma, kulikuwa na Gayo wengi. Kwa hivyo, hatuwezi kusema chochote kingine kuhusu mtu huyu zaidi ya tunachosoma katika barua hii. Na kuna habari nyingi za kutosha hapo, kama tutakavyoona. Mzee anampenda mtu huyu ambaye, katika hali ngumu ya kanisa, amesimama imara katika 'kweli', yaani upande sahihi wa nje ya mstari wa mgawanyiko.

Walimu sahihi njiani 3 Yohana 5-8

Maneno machache ya mzee yanatoa habari za kihistoria za thamani kubwa kuhusu makanisa ya mwanzo. Kulikuwa na kundi la walimu watembezi ambao walikuwa na msaada mkubwa wa mzee. Kwa wazi, Gayo alikuwa akiwakaribisha watembezi hawa, kuwatunza, na kuwasindikiza njiani. Hivi ndivyo mzee alivyojifunza, na alifurahi sana. Watembezi hao hawakufuata malengo yao wenyewe, wala hawakuomba chochote kwa ajili yao kutoka kwa mtu yeyote. Wanasafiri kwa ajili ya 'Jina', jina la Kristo (neno 'Kristo' liliongezwa na mtafsiri) na hawapati riziki yao kutoka kwa watu wa mataifa. Hivyo, wanafanya kama Paulo alivyofanya ambaye, kama 1 Wakorintho 9 inavyosema, hakutaka kuishi kwa gharama za watu wengine katika kazi yake ya injili.

Diotrefe na Demetrio 3 Yohana 10-11

Mzee sasa analeta sababu halisi ya kuandika barua. Tatizo ni mtu anayeitwa Diotrefe, ambaye kwa tafsiri halisi anasemwa 'anapenda kuongoza kanisa'. Lakini huyu si mtu ambaye anajitahidi tu kuwa kiongozi kanisani, bali ni mtu ambaye tayari yuko katika nafasi hiyo na anayetumia mamlaka yake kwa nguvu. Mzee ameandikia kanisa barua ya mapendekezo kuhusu watembezi anaowajua, lakini Diotrefe ameipuuza kabisa. Amepinga waziwazi mamlaka ya mzee na kuwakataa watembezi. Zaidi ya hayo, amewafukuza kanisani wale waliowapokea. Kwa hivyo, amefanya hasa kama 2 Yohana inavyoagiza lakini ametumia maelekezo hayo kwa watu wasiofaa. Ndiyo maana siku itakuja ambapo mzee atarudi kanisani na suala hilo litazungumzwa hadharani.

Tunaweza pia kwa urahisi kubainisha jukumu la Demetrio. Yeye ni aina ile ile ya mwalimu mtembezi ambaye Diotrefe ama amemkataa tayari au ambaye yuko hatarini kukataliwa. Lakini Demetrio anafanya jambo sahihi kabisa na ana ushuhuda mzuri si tu kutoka kwa Wakristo wengine bali pia kutoka kwa mzee – na kama inavyosemwa kwa njia ya ajabu, kutoka kwa Kweli yenyewe. Bado haijulikani jinsi Bwana alivyotoa ushuhuda huu wake.

Salamu za mwisho 3 Yohana 13-15

Salamu za mwisho zinafanana kwa kiasi na mwisho wa Waraka wa Pili wa Yohana. Hapa pia, maelekezo yaliyoandikwa ni mafupi sana na wazi, lakini hivi karibuni wataweza kuzungumza uso kwa uso na kwa utulivu. Hadi wakati huo, maelekezo yaliyotolewa sasa yatatosha. Katika hali ngumu, mzee anaomba kwamba rafiki zake wasalimiwe mmoja mmoja. Ingawa Diotrefe hangetambua mamlaka yake, watu wengine wengi walitambua, na wanahitaji kujua hali ilivyo. Yote haya yalikuwa kuhusu nini?

Kwa sehemu kubwa, ni rahisi kuelewa kilichokuwa kikiendelea, hata kama Gayo, Diotrefe, na Demetrio hawajulikani kwetu kwa njia nyingine yoyote. Hata hivyo, ni rahisi kiasi kuwaona katika nafasi zao. Diotrefe ni mchungaji wa kanisa, Gayo ni mwanakutaniko, na Demetrio kwa wazi ni mhubiri mtembezi anayekuja kwa Gayo na barua ya mapendekezo kutoka kwa mzee. Diotrefe hatawapokea walimu watembezi na anapinga waziwazi mamlaka ya mzee. Ikawa hivyo, mzee anampuuza Diotrefe na anamgeukia Gayo, mwanachama wa kanisa, akimhimiza awakaribishe watembezi licha ya kiongozi wa kanisa.

Muhtasari mkuu unaonekana wazi kabisa, lakini kisha maswali yanaanza. Je, Diotrefe anawakataa watembezi kwa sababu za kimafundisho au yeye ni mchungaji wa kanisa ambaye kwa ujumla yuko kwenye njia sahihi lakini anajiona tu? Ni vigumu kuamini kwamba ingekuwa suala la tofauti za tabia au kiu ya mamlaka tu. Ni vigumu zaidi kuamini wazo kwamba suala hilo lingekuwa kuhusu mifumo miwili tofauti ya kanisa inayogongana. Kwa wazi uwezekano mkubwa zaidi ni kwamba Diotrefe aliwakataa walimu watembezi kwa sababu za kimafundisho. Alikosea katika hili, na kwa hivyo hakuna mtu aliyepaswa kumtii.

Hatujui hatimaye mambo yalimalizikaje. Labda Diotrefe alishinda mwishowe na Gayo pia akafukuzwa kanisani. Hata hivyo, inawezekana pia kwamba nyumba ya Gayo ingeweza kutumika kama kituo kwa mzee na rafiki zake kulirudisha kanisa kutoka kwa Diotrefe. Angalau mtu fulani alijali kuhifadhi barua na kuinakili kwa vizazi vijavyo. Ni nani aliyefanya hivyo, kama si Gayo au mzee na kundi lake? Angalau tulijifunza kwamba hakuna mtu anayepaswa kumtii mchungaji wa kanisa ambaye yuko katika makosa.

Tunaweza kujifunza nini kutokana na haya?

Waraka wa Pili na wa Tatu wa Yohana unatuelezea hali mbili tofauti. Katika ya kwanza, kanisa liko kwenye njia sahihi, lakini watembezi wako kwenye njia mbaya. Katika ya pili, kanisa liko kwenye njia mbaya na watembezi wako kwenye njia sahihi. Tunatumia haya vipi katika wakati wetu na hali yetu?

Kanisa letu limetaka kuhifadhi mafundisho safi kwa njia ya kila mchungaji kujitolea katika kiapo cha kuwekwa wakfu kwa imani ya Kilutheri. Ni kazi ya maaskofu kulinda usafi wa mafundisho. Hii inakusudia kulilinda kutaniko ili wale wanaofundisha uzushi wasimpeleke mtu yeyote kwenye laana pamoja nao. Katika miongo ya hivi karibuni, hili limekuwa nadharia tu katika kanisa letu. Karibu mtu yeyote anaweza kufundisha karibu chochote kanisani. Labda kwa sababu hiyo hasa nyaraka hizi zina ujumbe wa wakati muafaka kwetu.

Kwanza, tulijifunza kwamba kwa kweli hatupaswi kuwapendelea walimu wa uongo. Hii ni rahisi kuona katika hali za wazi. Hatutawapokea Mashahidi wa Yehova au Wamormoni au kutoa nyumba yetu kama kituo kwao. Bado ni wajibu wa askofu kuhakikisha kwamba walimu wengine wanaopotoka kutoka neno la Mungu pia hawaalikwi kuhubiri katika ibada za kanisani. Hatutanunua vitabu vyao au kujiandikisha kwa majarida yao bali tutawakataa mara moja na kwa milele. Uzushi si jambo dogo. Kwa mtazamo wa Luther, ni jambo lile lile linalofanya jina la Mungu lidhihakiwe miongoni mwetu.

Pili, tulijifunza kwamba cheo rasmi hakimfanyi mtu yeyote kuwa asiyeshindika. Mchungaji na askofu wa kanisa wana kazi muhimu ya kulinda mafundisho ya kitume. Wakipotoka kutoka hapa, wanapoteza idhini yao. Hapo marufuku wanayoweka yanapaswa kupuuzwa. Walimu sahihi wanaotoka nje ya kanisa lazima wapendelwe hata kwa hatari ya kuishia kuitwa watu wa madhehebu na wazushi. Kwa hivyo, nafasi ya mtu kanisani si muhimu bali ni kujitolea kwa imani ya kitume. Haidhuru mtu yeyote anasema nini, kasisi aliye na makosa bado ana makosa, na mwanakutaniko wa kawaida anayekiri imani ya kweli bado yuko sawa.